HAWATOKI WATAKE WASITAKE.
Ushindi wa idadi yoyote ya mabao katika mchezo wa kesho dhidi ya Mbeya
City utakaochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya utaipa ubingwa Azam kwani
itafikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika ligi
hiyo.
HAWATOKI. Ligi Kuu Bara imefikia patamu huku Azam FC na Yanga
zikipigana kufa na kupona kutwaa ubingwa, lakini mechi iliyobeba gumzo
ni ile itakayochezwa Jumapili (kesho) kati ya Mbeya City na Azam huku
kila upande ukikataa kupoteza mchezo huo.
Azam chini ya Kocha, Joseph Omog ipo kileleni
katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 56 ikifuatiwa na Yanga yenye
pointi 52 na Mbeya City ni ya tatu ikiwa na pointi 46. Timu zote
zimecheza mechi 24 na kubakiwa na michezo miwili.
Ushindi wa idadi yoyote ya mabao katika mchezo wa
kesho dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya utaipa
ubingwa Azam kwani itafikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu
yoyote katika ligi hiyo. Yanga ikishinda mechi zake mbili itafikisha
pointi 58 tu.
VITA YA UBINGWA
Mechi mbili za kesho Jumapili kati ya Mbeya City
na Azam na JKT Oljoro na Yanga zitatoa picha ya ubingwa msimu huu
lakini, macho ya mashabiki wengi yatakuwa Mbeya katika mechi ya Azam na
Mbeya City.
Katika mchezo wa kwanza Novemba mwaka jana kwenye
Uwanja wa Chamazi, Mbagala Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya
mabao 3-3 huku zote zikiweka rekodi ya kutofungwa mchezo wowote katika
mzunguko huo.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Azam, Omog
alisema: “Kila mechi ni ngumu kwetu, lakini tutahakikisha tunashinda
mechi yetu ya Mbeya City na kutangaza ubingwa.
“Tumekuwa na malengo ya ubingwa kwa muda mrefu na Jumapili ndiyo siku yetu, tutapigana kwa nguvu zote ili tushinde.”
Lakini Kocha Msaidizi wa Azam, Kally Ongalla
alisema: “Mbeya City wana mashabiki wengi lakini wakumbuke kuwa
tumezifunga Simba na Yanga zenye mashabiki wengi kuliko timu zote za
soka hapa nchini.”
Beki wa kati wa Azam, Aggrey Morris alisema: “Tuna
kila sababu ya kuifunga Mbeya City na kutangaza ubingwa wetu, hatuwezi
kufanya mchezo juu ya hilo.”
Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi alisema:
“Mashabiki waje kwa wingi kuona mechi nzuri na ya ushindani, tumejipanga
kuicheleweshea Azam ubingwa. Hatutakubali kufungwa nyumbani kwetu.”
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe
amelalamikia proganda nyingi chafu zinazozushwa na baadhi ya watu katika
kuelekea mchezo huo ambazo siyo sahihi.
No comments