Azam FC haitaki shida yaufuata ubingwa kwa ndege Mbeya .
AZAM FC haitaki shida, kwani inaondoka leo Dar es Salaam kuja Mbeya kwa ndege ili kuhakikisha inafanya vizuri katika mchezo wake wa Jumapili (kesho) dhidi ya Mbeya City na kutangaza ubingwa.
Timu hiyo inayoshika nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, haitaki kuwachosha wachezaji wake na imeamua kutumia usafiri wa ndege ili wachezaji wasichoke na kushindwa kucheza vizuri katika mchezo wa kesho.
Azam imepanga kutengeneza rekodi mbili katika mchezo huo, kwanza kushinda na kutangaza ubingwa kwani itafikisha pointi 59 ambazo hata kama Yanga yenye pointi 52 ikishinda mechi mbili ilizobaki haitaweza kuzifikia, Yanga inaweza kufikisha pointi 58 tu.
Pili, Azam inataka kuvunja mwiko wa Mbeya City wa kutofungwa kwenye Uwanja wa Sokoine, tangu ilipopanda daraja msimu huu.
Mabosi wa benchi la ufundi na wachezaji wa Azam wote wanazungumza lugha moja ya ushindi dhidi ya Mbeya City hasa baada ya kuitandika Ruvu Shooting mabao 3-0 juzi (Alhamisi) katika Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Kocha wa Azam, Mcameroon, Joseph Omog alisema: “Kila mechi ni ngumu, lakini tutahakikisha tunashinda mechi yetu ya Mbeya City na kutangaza ubingwa.”
“Tumekuwa na malengo na mbio hizi tumekimbia kwa muda mrefu na Jumapili (kesho) ndiyo siku yetu, tutapigana kwa nguvu zote.”
Katibu mkuu wa Azam, Nassor Idrissa alisema: “Ni nafasi muhimu kwetu na tuna kila sababu ya kuifunga Mbeya City na kutangaza ubingwa.”
“Kama unavyojua, tukio la namna hiyo tumelifukuzia kwa kipindi ki kirefu na miaka miwili mfululizo tumemaliza katika nafasi tatu za juu, sasa ni jukumu letu kushinda mechi hiyo.”
Azam jana ilicheza mazoezi yake ya mwisho kwenye
moja ya viwanja vyake vinavyoendana na ule wa Sokine vilivyoko Azam Complex Chamazi, Mbagala Dar es Salaam ili iweze kucheza soka safi jijini Mbeya.
Mashabiki kadhaa wa soka kutoka Dar es Salaam na maeneo mengine jirani na Mbeya wameanza kuwasili jijini hapa kushuhudia mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki wengi.
No comments