OKWI AZUA UTATA MWINGINE YANGA.
Jamaa anapiga Sh6.4 milioni. Sasa ameibua utata mwingine ndani ya Yanga
ambao umemlazimisha kocha wake kumchimba mkwara mzito. Imebainika kwamba
Okwi haumwi chochote kama baadhi ya viongozi wanavyosisitiza.
BONGO kwa sasa kuna timu nne ambazo
zinalipa wachezaji mishahara ya maana. Kuna Yanga, Simba, Azam na
Coastal Union. Lakini timu zote hizo na wachezaji wote unaowajua
wachezaji huko hakuna ambaye anakula mkwanja mkubwa kama Emmanuel Okwi
wa Yanga.
Jamaa anapiga Sh6.4 milioni. Sasa ameibua utata
mwingine ndani ya Yanga ambao umemlazimisha kocha wake kumchimba mkwara
mzito. Imebainika kwamba Okwi haumwi chochote kama baadhi ya viongozi
wanavyosisitiza.
Mmoja wa vigogo wazito wa Shirikisho la Soka la
Uganda (Fufa), ambaye ni swahiba mkubwa wa mchezaji huyo aliyesusa
kuzungumza chochote, alisema alimwambia kwamba Yanga wamekiuka mkataba
wake ndio maana akasusa.
Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, anadai kwamba
Okwi hayupo katika kikosi hicho kutokana na kupata maumivu ya goti
lakini daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani, ambaye alisema hana taarifa
zozote za kuugua kwa mchezaji huyo aliyeigharimu Yanga na kusema
kutokuwapo kwake uwanjani kunatokana na matatizo ya kiutawala ambayo
hayajui wala hayamhusu.
Sufiani alisema katika faili lake kulikuwa na
wagonjwa wawili tu ambao ni kiungo Haruna Niyonzima na beki David
Luhende ambao hata hivyo wameshapona na jana Alhamisi jioni
waliotarajiwa kuanza mazoezi na wenzao kabla ya kuanza safari leo Ijumaa
alfajiri kuelekea Arusha kuifuata JKT Oljoro.
“Binafsi sina taarifa za kuumwa kwa Okwi,
kutokuwepo kwake kwenye timu siyo kwa sababu za kitabibu, ni matatizo ya
kiutawala zaidi ambayo siyajui wala hayanihusu, ” alisema Sufiani
ambaye ni daktari wa zamani wa Taifa Stars na Kilimanjaro Stars.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa,
ambaye alinogesha filamu hiyo kwa kusema tangu walipomaliza mchezo dhidi
ya Mgambo JKT wiki moja iliyopita na kuanza maandalizi ya mchezo
uliofuata, Okwi hakuonekana tena katika mazoezi huku akisisitiza
watafutwe viongozi ambao ndiyo wana majibu ya jambo hilo.
“Hatuna taarifa za kuumwa kwa Okwi, tunasikia tu
anaumwa mara ya mwisho tulikuwa naye Tanga alipocheza mchezo dhidi ya
Mgambo, alicheza vizuri na hakuwa na maumivu yoyote, sijui hayo maumivu
ya goti yamemuanza lini na aliyapata katika mchezo gani,” alisema Mkwasa
ambaye ni miongoni mwa makocha wasomi wa Tanzania.
Juhudi za kumtafuta Okwi zilifanyika kwa kiwango
cha kutosha lakini mchezaji huyo hakutoa ufafanuzi. Kocha Pluijm
alisema; “Siwezi kumzungumzia mchezaji asiyekuwapo pamoja na timu, suala
lake waulize viongozi wa juu ndiyo wanaoweza kulizungumzia kwa undani.
“Katika timu yangu hana nafasi ya kucheza, hata
kama akija kambini siku mbili au moja kabla ya mchezo hatapata nafasi
kwa sababu hajafanya mazoezi ya pamoja muda mrefu. Siyo huyo peke yake
hata hao wengine, mchezaji asiyefanya mazoezi ya pamoja na timu kamwe
sitampa nafasi.”
Okwi alikuwapo jukwaani Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam juzi Jumatano akifuatilia mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya
Kagera Sugar ambayo Yanga ilishinda mabao 2-1, lakini aliondoka robo saa
kabla ya mechi hiyo kumalizika.
No comments