Ngoma atinga anga za Mahrez, Chicharito Na whezron - May 17, 2016 250 0
NA MWANDISHI WETU
DONALD Ngoma kesho atashuka kwenye Uwanja wa Nelson Mandela
kuitumikia timu yake ya Yanga itakayokuwa ikipepetana na G.D Sagrada
Esperanca ya Angola, huku akiwa amefanikiwa kufanya kile kilichofanywa
na wakali wa mabao Ulaya kama Riyad Mahrez wa Leicester City ya England,
Javier Hernandez ‘Chicharito’ wa Leverkusen ya Ujerumani, Boria
Gonzalez wa Eibar ya Hispania, Carlos Bacca wa AC Milan ya Italia, Lucas
Martinez wa Deportivo La Coruna ya Hispania na wengineo.
Hadi sasa Yanga ikiwa imecheza mechi 29 za Ligi Kuu Tanzania Bara,
Ngoma ameshafunga mabao 17 msimu huu kama ilivyo kwa wakali hao katika
ligi wanazocheza.
Wakati ligi za Ulaya zikiwa zimeshafikia ukingoni, kule England,
Harry Kane wa Tottenham ndiye aliyeibuka kinara wa mabao kwa kucheka na
nyavu mara 25, huku Hispania mbabe wao akiwa na Luis Suarez wa Barcelona
mwenye mabao 40.
Huko Ujerumani, aliyefunga mabao mengi zaidi ni Robert Lewandowski
wa Bayern Munich (30), Italia ni Gonzalo Higuin wa Napoli (36) na
Ufaransa ni Zlatan Ibrahimovic wa Paris Saint-Germain (PSG) aliyetikisa
nyavu mara 38.
Hata hivyo, Ngoma anaweza kuongeza idadi ya mabao ya kufunga wakati
Yanga itakapoivaa Majimaji katika mchezo wao wa mwisho wa ligi Jumapili
hii kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Ngoma, pacha wake katika safu ya
ushambuliaji ya Yanga, Amissi Tambwe, hadi sasa amefunga mabao 21 ambapo
iwapo atatikisa nyavu zaidi ya mara tatu Jumapili dhidi ya Majimaji,
anaweza kufikia idadi ya mabao yaliyofungwa na
washambuliaji tishio Ulaya kama Jamie Vardy wa Leicester City mwenye
24, Edinson Cavani wa PSG (21), Lionel Messi wa Barcelona (26), Karim
Benzema wa Real Madrid (24), Neymar wa Barecona (24), Antoine Griezmann
wa Atletico Madrid (22), Pierre-Emerick Aubameyang wa Borussia Dortmund
na wengineo.
Ngoma na Tambwe wametoa mchango mkubwa katika kikosi cha Yanga na hatimaye kutwaa ubingwa wa Bara wakiwa na mechi tatu mkononi.
Mchezo wa Jumapili utakuwa wa mwisho kufunga msimu huu na hivyo kujiandaa na msimu ujao kutetea ubingwa wao kwa mara nyingine.
No comments