Tupashane Habari 24-hours

Tupashane Habari 24-hours

Breaking News

kampa kampa tena

Kessy vs Juma Abdul Mbona patachimbika


NA ZAITUNI KIBWANA
HAPANA shaka kwa sasa Juma Abdul, Hassan Ramadhan ‘Kessy’ na Shomari Kapombe ndio mabeki wa kulia bora nchini, wamethibitisha ubora wao Ligi Kuu Bara na hata katika michezo ya kimataifa ya timu zao na Taifa Stars kila walipopata nafasi ya kucheza.
Nani asiyejua uwezo wa Abdul, Kessy na Kapombe? Kwanini tusifananishe uwezo wao na nahodha wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil, Marcois Evangelista de Morais ‘Cafu’ au Danny Alves?
Uwezo wao wa kupandisha mashambulizi kwa timu pinzani, kucheza kwa kasi ya hali ya juu mwanzo mwisho kumewafanya  kuonekana kama ni beki mwenye mapafu ya mbwa.
Kimsingi naweza kusema kwa hivi sasa Tanzania kuna mabeki watatu wa kulia ambao wamemfanya kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa, kukenua meno kila mara aitapo wachezaji wa kuunda kikosi cha timu ya Taifa.
Uwezo wao wa kupandisha mashambulizi, kupiga krosi, kurusha mipira hizi ni sifa zinazoendelea kuwakosha mashabiki mbalimbali wa timu zao.
Baada ya kila mmoja kuwa kwenye himaya yake, Juma Abdul (Yanga), Kapombe (Azam) na Kessy (Simba) na kugombea namba wanapokutaka kwenye timu ya taifa tu, sasa mambo yamebadilika na Abdul na Kessy wamejikuta wakiingia kwenye vita mpya ya namba Jangwani.
Hii ni baada ya Kessy kusajiliwa Yanga akitokea Simba na moja kwa moja kuhamishia ile vita ya nani acheze kwenye kikosi cha kwanza cha Stars pale anapokosekana Kapombe katika makutano ya mtaa wa Jangwani na Twiga.
Kessy aliyesajiliwa na Simba akitokea kwa wakata miwa wa Turiani, Mtibwa Sugar amejizolea umaarufu mkubwa kwa muda mchache alioichezea Simba na hii inatokana na kiwango bora alichokionyesha licha ya umbo lake la kawaida.
Ni mchezaji mwenye pumzi ya kutosha na ni mzuri wa kukaba na kuipandisha timu mbele na ni mpishi mzuri wa magoli, sababu ambayo imepelekea mashabiki kumfananisha na nyota wa Barcelona, Dani Alves.
Tofauti na wachezaji wengi wa hapa Tanzania, Kessy anajiamini sana akiwa uwanjani na hata nje ya uwanja hakika kijana huyu ameitendea haki jezi yake namba 4 ambayo ameichagua kuivaa jezi ambayo imewahi kuvaliwa na wakali wengi waliopitia katika klabu ya Simba akiwemo mlinzi Victor Costa Nampoka.
Kutokana na uwezo wao kufanana wakiwa na timu zao, BINGWA leo linachambua uwezo wa wachezaji hao huku kwa upande wa Kessy na Abdul ambao sasa watakuwa kwenye timu moja.
Ni vyema tukaangalia vigezo muhimu vinavyoweza kutuongoza kuwalinganisha ili kufahamu ubora wao, labda mifumo ya timu zao nayo inafaa kuangaliwa kwani mara nyingi ndiyo inayomwelekeza beki nini afanye na kwa wakati gani.
Unapoiangalia Yanga inayopenda mfumo wa 4-4-2 unagundua kuwa mfumo huu unategemea sana viungo wa kati na pembeni kuwachezesha washambuliaji wa kati kujipatia magoli hapa ndipo unapopata picha kuwa mashambulizi ya Yanga hutengenezwa kutoka kwa Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Geofrey Mwashiuya, Deus Kaseke na Malimi Busungu na hivyo Yanga hawategemei sana krosi za mabeki wa pembeni labda itokee tu.
Kwa hali hiyo, Juma Abdul hana fursa nyingi zinazomsogeza karibu na goli ili azitumie na kufunga isipokuwa kwa kutumia uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali kufunga magoli, ingawa nafasi hizo hazitokei mara kwa mara na kumwacha ategemee mipira ya adhabu kubwa.
Katika ulinzi itakuwa rahisi kwake kuihami timu vizuri, muda mwingi haondoki katika nafasi yake isipokuwa kwa nadra.
Asilimia kubwa ya magoli ya Yanga yanatengenezwa upande huo na pia ana uwezo mkubwa wa kupiga mashuti na krosi. Ukiachana na michezo ya ligi kuu, Abdul ameonyesha kiwango maridhawa katika mechi ngumu za kimataifa mwaka huu!
Hakika vijana hawa wamejitahidi sana na kuonyesha kuwa wanaweza kuja si kuziba tu ile nafasi ya Nsajigwa katika timu ya taifa, bali kuifikisha mbali zaidi timu yetu ya Taifa ya Tanzania na hususani klabu zao.
Kwa Kapombe sote tunaweza kukumbuka aina yake ya uchezaji kama mlinzi alipokuwa Simba, alitumia muda mwingi kukaba na muda mchache kushambulia hata mabao yake ya kufunga yalikuwa machache.
Wakati Kapombe inapobidi kukaba anafanya hivyo kwa bidii na uwezo mkubwa. Kwa sasa si rahisi kwake kuonekana hivyo kama zamani kutokana na mfumo wa Azam wa 3-5-2 huku yeye akipewa uhuru (Free role) kunyatia matundu yanayojitokeza ndani ya eneo la hatari la timu pinzani, kuiwahi mipira inayozagaa na hivyo kufunga magoli muhimu kwa timu yake ambayo huenda yakamfanya aweke rekodi ya beki aliyefunga mabao mengi katika ligi yetu na ligi zote za ukanda huu wa Afrika, manane (8) hadi sasa.
Lakini wakati Kapombe akitakata kwenye mfumo wa 3-5-2, ni wazi kuwa Kessy na Abdul wataendelea kutumika kwenye mfumo wa 4-4-2 ambao hupendwa zaidi na kocha Hans van der Pluijm.
Kessy na Abdul wote wana sifa ya kupandisha timu na kushiriki kwenye kutengeneza nafasi na ndiyo maana Abdul amehusika kwenye sehemu kubwa ya mabao ya Yanga na ndivyo hivyo hivyo Kessy amefanya kwenye kikosi cha Simba.
Tafauti pekee kati yao hasa kwenye idara ya kushambulia ni ukweli kuwa Abdul huwa ana maamuzi mazuri zaidi ya mwisho kuliko Kessy ambaye wakati mwingine huonekana kukosa umakini na kushindwa kumalizia vizuri kazi kubwa ambayo anaweza kuwa ameifanya.
Na ndiyo maana Juma Abdul amekuwa mfungaji mzuri zaidi ya Kessy kwenye msimu huu hii ni kutokana na utulivu wake anapokuwa mbele na mpira.
Lakini ukirudi kwenye idara ya ukabaji ni wazi kuwa wote ni mabeki wazuri na wenye uwezo mkubwa sana kwa kukaba, ila kwenye idara hii siku zote Kessy ni bora zaidi ya Juma Abdul kitu kinachomfanya kuwa bora sana akiwa uwanjani pale timu inaposhambuliwa.
Watu bado wanajiuliza watachezaje vijana hawa wawili kwenye timu moja, lakini si ajabu Pluijm akaamua kumsogeza mmoja mbele kucheza kama winga kama ambavyo Jackson Mayanja alikuwa akimtumia Kessy wakati mwingine alipokuwa Simba.
Hivyo, huwezi kukosea ukisema Pluijm ndiye anajua atawatumiaje hawa mabeki wawili, lakini kiukweli Kessy vs Abdul mbona patachimbika!

No comments