Stewart Hall alia na wachezaji wake
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema ni kama `waliporwa’
ushindi na Ndanda FC katika mchezo wa juzi baada ya wachezaji wake
kushindwa kutimiza ipasavyo majukumu yao uwanjani. Katika mchezo huo
uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Azam FC ililazimishwa
sare ya mabao 2-2.
Timu hiyo ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 kipindi
cha kwanza cha mchezo huo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lakini ilijikuta
ikiondoka na pointi moja baada ya Ndanda kusawazisha mabao yote kipindi
cha pili. Akizungumza juzi baada ya mchezo huo, Hall alisema wachezaji
wake hawakujiamini mchezoni na walikosa ari ya kupambana ili kusaka
ushindi.

“Hatukucheza
vizuri kabisa, tulicheza vyema dakika 20 za mwanzo na baada ya hapo
hatukuuonesha mchezo mzuri hasa kipindi cha pili, nadhani leo (juzi)
wachezaji walikosa kujiamini na kutimiza majukumu yao uwanjani,”
alisema.
Alisema kila mtu anajisikia furaha kulaumu waamuzi na
wengine, lakini wakati huo wachezaji walishindwa kutimiza majukumu yao
na hiyo imeonekana hata kwenye mechi zao mbili zilizopita.
Azam FC
imefikisha pointi 52 na kubakia katika nafasi ya tatu, huku ikizidiwa
pointi moja na Yanga inayoshika nafasi ya pili na pointi tano dhidi ya
Simba iliyo kileleni, lakini imeizidi Yanga mchezo mmoja huku ikizidiwa
mechi moja na Simba.
No comments