Inawezekaje wasanii kujiita kioo cha jamii kwa Tungo zilizojaa matusi?
Inawezekaje wasanii kujiita kioo
cha jamii kwa Tungo zilizojaa matusi?
Na Abdiel Sifi, OUT
Sanaa ya
muziki Tanzania ina historia ndefu, ukichunguza kuchimba na asili yake.
Muziki
na wasanii wamepitia mabonde na milima. Kabla
ya uhuru, baada ya uhuru, na wakati huu wa sayansi na teknolojia ya mawasiliano
inayochanua kwa kasi. Ndivyo vipindi iliyopitia sanaa ya muziki na ilipo sasa.
Yafaa
kuelewa neno Mwanamuziki maana yake.Mtu mwenye uwezo wa kuimba, kutunga mashairi,
kutumia vyombo vya muziki, kucheza nk. Ingawa si lazima kwa mtu kuwa na uwezo
katika nyanja zote hizo.Aghalabu ajue kutumia moja wapo ya chombo cha muziki kama kupiga ngoma,
filimbi, gitaa, Tarumbeta nk.
Haileti
mantiki mtu kuitwa mwanamuziki ili hali hajui kutumia hata chombo mojawapo cha
muziki. Haiwezekani mwanajeshi akaitwa mwanajeshi kwa kuvaa sare tu, bila
kupitia mafunzo ya jeshi, kutumia silaha,Mpaka awe amepitia mafunzo ndipo huitwa
Mwananajeshi, muziki pia inatakiwa hivyo.
Muziki
wa tangu uhuru,mfumo wa vyama vingi, hadi leo unatoafautiana sana katika
uimbaji, utunzi wa mashairi, upigaji na maudhui yake.
Wasanii
wa kitambo muziki wao ulilenga kuelimisha jamii, kuburudisha, kuonya, kukemea,
kutoa tahadhari, lakini maisha yao hayakuwa na hadhi kama wanamuziki wa leo.
Tofauti
na sasa ambapo msanii anaimba matusi,
kejeli, dharau, kujisifu,akiwa hawezi kutumia chombo chochote cha muziki na kudiriki kujiita
Mwanamuziki, ingawa hajui kupiga ngoma ambayo ni asili ya makabila ya Kitanzania.
Makala
haya yanalenga kujadili zaidi Maudhui ya nyimbo zinazoimbwa kila siku na
wasanii wanaoongezeka kama uyoga ulioota kwenye pori la rutuba nyingi.
Haipiti
siku bila kusikia wimbo na msanii mpya akichomoza. Hata hivyo nyimbo na wasanii
wanaochomoza gizani na kuangaza kwa muda tu, nyota zao huzimika kama moto wa
mshumaa. Kuzimika kwao kuna sababu mbalimbali ikiwa kutunga nyimbo zisizosadifu
maadili ya kitanzania ,utamaduni na hali ya maisha halisi ya Kitanzania.
Kwa mtu
mwenye busara na maadili inamuwia vigumu kukaa kitako na watoto wake, kuangalia
video ya bongo flava, kutokana na maudhui na picha zinazoonekana kujaa matusi,mapenzi
kejeli na dharau.Itamlazimu haraka kubadili kituo,kisa! Wimbo umesheheni matusi, dharau,
kejeli. Nk.
Sio siri
nyimbo, video za bongo flava zimejaa matusi, majigambo na mapenzi, ambapo
wasanii hujisifia wao na wapenzi wao ilihali wazazi (jamii) ina hali ngumu ya maisha, afya duni, ujinga,elimu
duni,njaa, maradhi, ufisadi nk. Sina lengo la kuwaelekeza vitu vya kuimba la
hasha!.Msanii ni kioo cha jamii ndio wanavyosema wao.Ikiwa hivyo kwanini wanashindwa kutazama jamii yao, kujua na
kutambua mahitaji yanayoikabili jamii
yao?
Hapo
nyuma wanamuziki waliimba nyimbo za kuelimisha jamii, kuonya na kukemea uvivu, ujinga,
kuchochea bidii kwa vijana, kujitambua, kupenda nchi yao (uzalendo) kuhamasisha
utalii na utunzaji wa mazingira.
Tuangalie
nyimbo chache kati ya nyingi zenye maudhui adhimu kwa jamii.Wimbo Dr Remi Ongala unaitwa Tanzania, una mashairi haya “mwaume
ni kilimo,mwanaume ni jembe, lima vizuri watoto wako watashiba, mke wako
hataombaomba”.Wimbo unahimiza watu
kufanya kazi kwa bidii (kulima) ili kuepuka njaa katika familia. Na ikiwa
wanaume wote watafanya hivyoTanzania itajikwamua katika njaa, umaskini yaani Tanzania
hitakuwa omba omba.
Wimbo wa
Baraka Mwishehe unaoitwa mama watoto,
anasema “baba watoto nashindwa nyamaza naona mambo yananitatiza,
tabu na raha ndio hali ya dunia lakini tabu nyingine tunajitakia”.Mashairi
yanatoa tahadhari juu ya nidhamu ya matumizi ya mali nyumbani. wanaume kuchukua
tahadhari katika familia. “Mwenzangu Weka
akiba”.Elimu juu ya watu kutambua wajibu kwa familia, malezi bora kuweka
akiba,kwa ajili ya watoto,ndiyo ujumbe uliochagizwa hapa.
Juwata
band na wimbo wasia kwa watoto. “Wakati wa ujana wangu, mimi baba yenu, shati
dukani shilingi sita dukani unapata, kwa sasa shilingi sita haupati hata mkate/soda.
Kuishi kupatana na wakati, jiepusheni na anasa, fanyeni kazi kwa bidii, kama
kuna mkorofi kati yenu aache mara moja”. Hakika hawa wazee walieneza elimu, nasaha murua kwa
vijana kuhusu maisha yanavyobadilika. Tahadhari, kuwa makini na muda na
kujitambua kutimiza wajibu wa kijana katika maisha.
Linganisha
na mashairi ya Nay wa Mitego nakula
ujana, wananita popo nakesha nakula ujana, kujirusha daile sina wikiendi.leta
pombe akimwaga tena tumgonge, na demu wake tumuibe. Nataka mademu mabonge
wemamba nimewapa likizo.
Mashairi
ya wimbo huu yanahamasisha vijana kutumia pesa ovyo bila kujali. Yanachochea
vijana kuendekeza starehe badala ya kazi.
Tazama video ya wimbo huu kwa makini, utawaona, hao
wanajiita wasanii kioo cha jamii, wakinywa pombe, wanamwaga, pembeni kuna dada
zetu waliobarikiwa na Mungu wamevaa chupi wakimshikashika Nay Wa Mitego huku
wakiwa katika furaha ya ajabu.
Swali la kujiuliza
ni busara watanzania kuonesha uchi wao hadharani? Je Baraza la sanaa
kazi yao ni nini? Video hizi zilizokosa maadili na staha hawazioni? Miaka kadhaa
baadaye kutakuwa naTaifa lenye watu wa maadili ya namna gani?
Hotuba ya uzinduzi wa Jamuhuri ya Tanganyika tarehe
09.12.1962, Mwalimu
Julius Nyerere,pamoja na masuala mengine, aliongelea
kuhusu historia ya
utamaduni wa Tanganyika.
“Nchi isiyokuwa na utamaduni
wake haina tofauti na mkusanyiko wa watu ambao
hawana roho iwawezeshayo kuwa
taifa”. Alivilaani vitendo vya wakoloni vya
kuwafanya Waafrika waamini kwamba
hawana utamaduni wao wenyewe; ama kuufanya utamaduni
wa Kiafrika uonekane
kitu cha ovyo.
Kutokana na hili, wengi wa waliokuwa wamesoma na
kupata elimu ya
Kizungu waliojiona kuwa ni “wastaarabu” walijifunza
kuwaiga Wazungu kiasi
kwamba kuwa Mwafrika msomi kulimaanisha kuwa Mzungu
Mweusi. Suala la
muziki, kama nyanja muhimu ya utamaduni katika
historia ya Tanzania, limekuwa
ainisho muhimu la migogoro ya kitamaduni.
Mwalimu
Nyerere katika hotuba hiyo alizungumzia juu ya elimu ya kikoloni, kwamba waliopata elimu hiyo
walifunzwa kuimba nyimbo za Kizungu,
lakini siyo za Wahehe au Wanyamwezi. Walifunzwa kucheza“rumba”, “chachacha”,
“rock ‘n’roll”, “twist, “waltz” na “Foxtrot”. Lakini wengi
walikuwa hawajawahi kucheza au hawakujua chochote
kuhusu “Gombe Sugu”,
“Mangala”, “Nyang’umumi,”
“Kiduo”, “Lele Mama”, au
“Mganda.” Wengi wa
waliosoma wakati wa ukoloni walijua kupiga gitaa au
piano, lakini walikuwa hawajui
kupiga
ngoma.
Haya
yalitamkwa 1962, wakati ambapo kulikuwa hakuna mitandao ya kimawasiliano, video
wala televisheni, kama ilivyo leo hii.Pamoja na mandeleo haya muziki waTanzania
umepoteza dira, kupotea kwa utambulisho wa muziki wa kitanzania kama sehemu ya
utamaduni. Badala yake wasanii huimba matusi, kujisifu na kujifananisha na
wazungu, ambapo kweli yake haimo.
Kwa ujumla
zipo nyimbo nyingi za wanamuziki wa zamani ambazo kusudi lake lilikuwa
kuelimisha jamii,kuburudisha, kutahadharisha.Wanamuziki walijua kutunga
mashairi yenye ujumbe murua, walijua kupiga vyombo vya muziki. Mpaka leo nyimbo
hizo zikipigwa utatingisha kichwa ishara kuwa unaridhika na mashairi au upigaji
wa vyombo vya muziki.
Leo
muziki umejaa matusi, unaoshabikia uzembe kwa vijana, kupenda starehe, anasa,
ili hali vipato vyao haviwezi kumudu
hali hiyo. Wasanii ni wasanii kweli, waongo, wanaigiza maisha ya uongo. Usasa
umetawala. Tukumbuke kuwa muziki ni sehemu ya utamaduni wa Taifa.
Tazama
muziki wa kihindi,kijamika,kibrazili kongo Kinshasa nk, ni muziki wa asili yao.
Vipi kwetu. Asili ya muziki wa kitanzania ni ipi? Mungu ailaze roho ya Bi Kidude
aliyekuwa Mwanamuziki mashuhuri Afrika mashariki. alitangaza muziki wa asili ya ukanda wa Pwani nje ya Afrika na
alipendwa na kuheshimika kitaifa na Kimataifa.
Licha ya
udhaifu wa maudhui ya nyimbo za bongo flava, muziki unazidi kupoteza asili na
utamaduni uliojaribiwa kujengwa miaka ya 1961/90.Sababu ni kuiga na kuchanganya
kila kitu kutoka kwa wengine na kuacha vya kwetu.
Nyimbo
za wasanii wa leo kama nilivyosema awali zimajaa matusi, mapenzi, zinazoshabikia
uzembe, ujinga. Haumfundishi mtoto
chochote,Kibaya zaidi watoto wanasikiliza na kuzikariri nyimbo hizi mpaka mwisho, kumzidi hata mtunzi, kuliko
kukariri masomo achilia mbali kuelewa. Miaka mitatu iliyopita baraza la mitihani lililamika
wanafunzi kuandika mistari ya nyimbo za
bongo flava wakikujibu mtihani wa kumaliza kidato cha nne.Si dalili nzuri,
kizazi kinapotoka, hatua mathubuti zinahitajika kuondoa uozo huu.
Hayo
ndiyo matokeo ya muziki wa bongo flava, umewaingia watoto ubongoni na kuwageuza magogoi, mbumbumbu, wajinga wasio
na fikira, waliokata tamaa,wasio na adabu, maadili,utii ujasiri,waoga,waliokosa
uzalendo kwa nchi yao.
Wasanii
fikira zao wamezielekeza katika mapenzi zaidi, bila kuelewa jamii inakabiliwa
na changamoto nyingi zinzohitaji kukemewa,na kutahadharisha jamii. Magonjwa,
rushwa na ufisadi ni baadhi yake.
Wasanii
wachache wanaothubutu kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira, mali
asili, nidhamu kwa watoto, na kuhamasisha utalii wa ndani na wa nje kama
alivyofanya mwanamuziki Nguli Baraka mwishehe kwa wake wimbo unaitwa watalii. Anasema, Tanzania ndio nchi peke yenye wanyama wengi wa kuvutia, watalii kutoka
ng’ambo mwakaribishwa mje kuona mengi mnaporudi kwenu mkasimulie.
Hakika
muziki wa Mwishehe ulijaa mafundisho kwa
watu wote, kuitangaza nchi yetu,mbuga za wanayama na mali asili alizisifu na
kutoa hamasa kwa wananchi kutambua umuhimu wa mazingira asilia. Kupenda nchi,
na kutahadharisha vijana kuwa na maadili mema.
Wakati
maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano yanaendelea kuchipua matawi kwa kasi
hapa kwetu, ni vyema mamlaka husika y usimamizi wa sanaa ya muziki (BASATA),
ikawasha sigara isiyozimika ili kumulika maudhui ya nyimbo za bongo flava.
Kinachokubalika
ni kwamba muziki wa bongo flava umekuwa ajira kwa vijana, unawapatia mafanikio
makubwa kimaendeleo.Wakati wakiendelea kusherehekea maendeleo yao ni vyema
wakajua kuwa Taifa na jamii linawatazama kama nguzo muhimu kujenga maadili na
kuipa mwelekeo jamii yao.
Mamlaka
na jamii inapofumba macho halafu wakisiliza na kushabikia mambo ya kijinga ni
wazi kuwa tumepoteza dira na tumeshindwa kuhifadhi asili na maadili ya kijamii.
Video za bongo fleva zinazokinzana na maadili ni
muhimu pia kumulikwa, ili zile zinazosadifu uongo, ujinga, ngono, na tamaduni
za nje zikachukuliwa hatua, ikiwemo kufungiwa na faini. Kama hilo haliwezekani
basi mamlaka husika itangaze kwa umma mchana kweupe kwamba “Tanzania ni nchi
isiyokuwa na utamaduni wake na ni mkusanyiko wa watu ambao hawana roho
iwawezeshayo kuwaTaifa”.
Makala haya Yameandikwa
na Abdiel Sifi
Kwa msaada wa Mtandao
E- mail dodisifis@yahoo.com
simu 0682 102 671
No comments