HATA KABLA YA GOLI LAKE DHIDI YA AZAM TAYARI JUMA ABDUL AMETHIBITISHA YEYE NI BORA
Na Baraka Mbolembole
Mlinzi wa kulia wa Yanga SC, Juma Abdul, siku ya Jumamosi iliyopita
alifunga goli la kusawazisha wakati timu yake ilipokuwa nyuma kwa goli
1-0 dhiya Azam FC. Juma alifunga kwa kiki kali ya mbali na bao lake hilo
limekuja baada ya kiwango cha juu kwa muda wa mwaka mmoja sasa.
Akiwa amechangia magoli mengi ya timu yake akicheza kama mlinzi wa
kupanda na kushuka katika fullback namba 2, Juma ni kati ya wachezaji
ambao wanastahili kupewa mkataba mpya wenye maslai zaidi kwenye klabu ya
Yanga ama nje ya timu hiyo.
Mlinzi huyo wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, alijiunga na Yanga,
Julai, 2012 akitokea Mtibwa Sugar na hadi sasa tayari ameshinda mataji
mawili ya VPL na moja la klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ( Kagame
Cup)
2012-2014
Hadi anamaliza mkataba wake wa awali wa miaka miwili klabuni Yanga,
Juma hakuwa mchezaji staa lakini kocha Ernie Brandts aliendelea kumjenga
mchezaji huyo licha ya kuwa chaguo la pili nyuma ya Mnyarwanda, Mbuyu
Twite. Juma alitumia vizuri kila nafasi iliyokuja mbele yake.
Mara kadhaa nilimsisitiza kutokubali kupoteza ari yake, nilicheza na
Juma katika timu ya vijana ya Kingalu Kids pale Morogoro, siku zote
alitaka kuwa mchezaji bora, ni mtu anayejituma sana, ana nidhamu,
msikivu, mvumilivu.
Katika msimu wake wa pili, kuna wakati nilimwambia ‘anakaribia kuwa
beki 2 bora Tanzania’ licha ya kwamba hakuwa mchezaji anayetazamwa sana
na mashabiki.
Alifikia uamuzi wa kuondoka klabuni hapo kama tu asingepewa mkataba
wenye maslai ya juu. Mkataba wake wa kwanza Yanga haukuwa na maslai ya
juu sana lakini kutokana na umri wake wa wastani nakumbuka nilimwambia
Juma asiondoke Yanga na badala yake azungumze nao vizuri kisha asaini
mkataba mpya bila kutazama maslai kwanza.
Juma hakuwa mchezaji wa timu ya Taifa (taifa stars) na wala hakuwa
mchezaji mwenye uhakika sana katika kikosi cha kwanza cha Yanga, na kwa
mchezaji kijana mara zote hapaswi kushindwa Yanga kwa sababu za
kimaslai. Juma alisaini tena mkataba wa miaka miwili kuendelea kubaki
Yanga.
2015-16
Amejitolea kwa nguvu zake zote, uwezo wake wote, jitihada zote na
sasa kikosi cha Hans Van der Pluijm kinaweza kucheza bila uwepo wake,
lakini si kwa tabia ya mashambulizi inayotumika kuanzia Januari, 2015
baada ya Hans kuchukua nafasi ya Mbrazil, Marcio Maximo mwishoni mwa
mwezi Disemba, 2015.
Mkataba wa Juma na Yanga unakwenda kumalizika baada ya kumalizika kwa
msimu. Nadhani Yanga wanapaswa kufanya haraka kumsaini tena mchezaji
huyo na si kufikiria kuwasaini wachezaji wapya. Wanapaswa kumuuliza Hans
kama ataendelea kumuhitaji Juma.
Hata kabla ya goli lake dhidi ya Azam FC tayari Juma amejithibisha
yeye ni mchezaji muhimu katika timu ya Yanga, amepewe mkataba mpya wenye
maslai sasa.
No comments