Tupashane Habari 24-hours

Tupashane Habari 24-hours

Breaking News

kampa kampa tena

KARUME MWANZILISHI WA YANGA NA JINA LA SIMBA SPORTS CLUB

HISTORIA yetu katika mambo mengi imepotoshwa ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya.Ni upotoshaji wa historia mtu anapoizungumzia klabu ya Young Africans maarufu kama Yanga bila kumzungumzia hayati Sheikh Abeid Aman Karume ambaye tangu atutoke kwa kupigwa risasi mwaka 1972, tarehe 7 mwezi huu na mwak huu ilitimia miaka 38 kamili.Ni upotoshaji wa historia mtu anapozungumzia jina la Simba Sports Club bila kumtaja Rais huyo wa kwanza wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza, wa kwanza, wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha,ni kosa kubwa kiimani na kimaadili mtu kuzipongeza klabu za Simba na Yanga kuwa na majengo yake bila kumhusisha kwa kiwango kikubwa hayati Karume.Kutomhusisha huko,kiimani ni dhambi ambapo kimaadili ni utovu mkubwa wa shukrani.Kwa maneno mengine,klabu za Yanga na Simba zilifanyiwa makubwa mno na hayati Karume kinyume cha jinsi historia inavyofanyiwa jitihada kwa Mwenyekiti huyo wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar kutosikika sana ndani ya klabu hizo za soka zenye mashabiki wengi ndani ya Jamhuri nzima ya Muungano wa Tanzania.

Aliyoyafanya Karume kwa Yanga

Historia iliyoandikwa haielezi vizuri ukweli kwamba Sheikh Abeid Aman Karume alikuwa mhamasishaji mkubwa wa kuanzishwa kwa klabu ya soka ambayo sasa ndiyo hii inayoitwa Young Africans yaani Yanga.Baada ya kufanya kazi ya ubaharia iliyomuwezesha kuzunguka karibu dunia nzima kwa miaka kadhaa akiwa kijana mdogo, Karume alipata uzoefu wa yaliyotokea kwenye nchi mbalimbali alizozunguka duniani na kugundua kwamba serikali za kikoloni zilipiga vita uanzishwaji wa vyama vya siasa na wananchi wazawa lakini zilikuwa hazipingi vyama vya kijamii kama klabu za michezo.

Baada ya kuufahamu ukweli huo,akiwa nyumbani Zanzibar,Karume alijiunga na wenzake na kuunda klabu ya soka iliyojulikana kama African Sports Club,mwenyewe akiwa mchezaji mahiri wa timu ya klabu hiyo.Humo humo kwenye mikutano ya kisoka ndimo yeye na Wazanzibari wenzake walikuwa wakijadili jinsi ya kujinasua toka kwenye utawala wa kisultani uliokuwa ukilindwa na Waingereza.

Ni hayati Karume ndiye aliyehamasisha kuanzishwa kwa matawi ya hiyo African Sports ya Zanzibar na akafanikiwa kuanzishwa kwa tawi la timu hiyo jijini Dar es Salaam ambalo kwa sasa ndilo hii klabu kubwa sana ya Yanga na kule Tanga alifanikisha kuanzishwa kwa tawi jingine ambalo ni African Sports ya Tanga.Kumbuka kuwa kwenye miaka hiyo ya nyuma miji ya Dar es Salaam,Bagamoyo,Pangani na Tanga ilikuwa na ukaribu sana wa kimahusiano na miji ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Baada ya kuanzishwa,timu hizo tatu za Yanga ya sasa,African Sports ya Zanzibar na African Sports ya Tanga zilitengeneza undugu wa damu mkubwa mno.Zote tatu zilikuwa chimbuko la hayati Karume ingawa historia haiuweki wazi ukweli huo.

Kwa Yanga pia, hayati Karume ndiye alitoa kiasi kikubwa cha pesa,kama siyo chote, mwaka 1971 kwa kufanikisha ujenzi wa jengo la makao makuu ya Yanga la sasa lililopo kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani,Kariakoo jijini Dar es Salaam.Alifanya hivyo kwa Yanga baada ya kushirikiana na wana Simba kupata jengo lao kwenye mtaa wa Msimbazi,Kariakoo,jijini Dar es Salaam mwaka huo 1971 kwa kuchangia kiasi cha pesa. Ki msingi,hayati Karume alishiriki kujenga majengo yote mawili ya klabu za Yanga na Simba ingawa historia iliyoandikwa haitaki kuuweka wazi ukweli huo.

Hivyo ndivyo hayati Karume alivyoifanyia klabu ya Yanga tangu kuanzishwa kwake mpaka kupata jengo la makao makuu yake.Ukitaka kuamini jinsi jengo la Yanga lilivyo na mahusiano na Wazanzibari,tangaza leo kupigwa kwake mnada,uone jinsi utakavyoshukiwa kwa hasira na Wazanzibari.Kama huamini,nitakukumbusha.Mwaka 1988 jengo hilo lilikuwa lipigwe mnada baada ya Yanga ya kina Ally Bwamkuu kudaiwa kiasi fulani kikubwa cha pesa.Kila kitu kilikamilika kwa hatua hiyo kutekelezwa lakini hilo halikufanyika baada ya jopo la Wazanzibari kadhaa kutia timu Dar es Salaam na kuweka pingamizi dhidi ya hatua hiyo kwa sababu kulikuwa na mkono wa Wazanzibari kwenye ujenzi wa jengo hilo.Mnada haukuwepo na deni lililipwa kwa njia nyingine.

Aliyoyafanya Karume kwa Simba


Kwa upande wa Simba iliyoanzishwa toka kwa watu waliojitenga toka klabu iliyoanzishwa kwa hamasa ya Karume iitwayo sasa Yanga,hayati Karume alifanya mambo makubwa pia.Siku ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la klabu hiyo la mtaa wa Msimbazi,Karume alitoa mchango wake wa fedha wa kufanikisha ujenzi wa jengo hilo. Hapo hapo alitoa rai kwa klabu hiyo kuachana na jina la Sunderland Sports Club lililokuwa likitumiwa na klabu hiyo hadi wakati huo.

Hakuishia kuelekeza tu kwamba jina hilo lilikuwa haliakisi utamaduni wetu na lilikuwa mwendelezo wa mabaki ya ukoloni bali pia alipendekeza jina linalotumika sasa na klabu hiyo nami nakumbuka wazi wazi nilivyomsikia akisema kupitia Radio Tanzania Dar es Salaam.Nakumbuka kumsikia akisema "Achaneni na jina hilo la kikoloni la Sunderland,kwani tuko Uingereza hapa? Mnaweza mkajiita Simba Mwekundu Sports Club,jina linaloeleweka na linaloendeana na utamaduni wetu..." Alipendekeza jina la Simba Mwekundu kufuatia rangi kuu ya klabu hiyo.

Wazo hilo likachukuliwa moja kwa moja na mwanzoni kutoka jina la Sunderland,kweli Simba ilikuwa ikiitwa Simba Mwekundu lakini baadaye ndipo ilipoandikishwa kama Simba Sports Club,jina alilolitoa hayati Karume kwa mdomo wake kabisa nami nikimsikia kwani mwaka 1971 nilikuwa mvulana wa shule ya msingi na sikuwa mdogo sana.Inasikitisha sana siku niliposoma mahali mdau mmoja wa Simba akisema jina hilo walilibuni wana Sunderland wenyewe baada ya Serikali kupiga marufuku majina ya vyama fulani vya nje.Hapana,huo ni upotoshaji wa dhahiri wa Historia,jina hilo lilitengenezwa kichwani mwa hayati Karume.Kama kweli Simba wenyewe waliliteua jina hilo kuwa lao badala ya Sunderland,basi tukubaliane kwamba uteuzi huo ulifanywa katika kurasmisha mapendekezo aliyoyatoa hayati Karume.

Kwa msingi ulio sahihi wa historia ya Yanga na Simba,hayati Karume anaweza kutajwa kuwa ndiye aliyezifanya klabu hizo ziwepo leo,ndiye aliyeshiriki moja kwa moja kuzipatia majengo wanayonufaika nayo leo na ndiye aliyeasisi jina la Simba Sports Club.Kama ilivyoelezwa,Simba ilianzishwa toka ubavuni mwa Yanga iliyoanzishwa kwa uasisi na ushawishi wa hayati Karume mwaka 1928 akiwa na umri wa miaka 23. Baadhi ya watu toka klabu hiyo moja walijitenga mwaka 1936 na kuanzisha klabu hii inayojulikana sasa kama Simba Sports Club.Ni kutokana na maelezo hayo ya kweli ya kihistoria ndipo unapoweza kumuweka hayati Abeid Aman Karume katikati ya uanzishwaji wa klabu zote za Yanga na Simba na unaweza pia kumuweka katikati ya mipango yake mikubwa ya maendeleo kama kumiliki majengo ambayo yanafaa kutumika kama vitega uchumi vya klabu hizo.

Ninamaliza kwa kutoa maombi manne.Kwanza,kwenye siku ya Karume Day ni vizuri tukimkumbuka Mwanamapinduzi huyo kwa kuwaeleza vijana makubwa aliyoifanyia nchi hii si kisiasa tu na kiuchumi bali pia kijamii kama nilivyofanya leo kuonyesha mchango wake kwa klabu za Yanga na Simba.Si vizuri watu kupumzika tu na kusema kuwa leo ni siku ya kumbukumbu ya tarehe aliyouwawa Karume,kwani kuuwawa kwa kiongozi wetu huyo kuna nini cha kutufanya tuitukuze siku hii? Mantiki ya kuifanya siku hii kuwa kuu ni kukumbushana kwa maandiko,kwa utangazaji na kwa makongamamo kuhusu mchango wa kiongozi wetu huyo kwa maendeleo yetu yakiwemo ya klabu za Yanga na Simba.

Pili,naomba jamii ya wapenda soka wa nchi hii iwe inaandaa mechi kubwa tu kwenye siku hii zenye sura ya Muungano wetu alioshiriki kuuasisi.Kunaweza kuwepo mechi ya kirafiki ya Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes au timu mchanganyiko ya Dar es Salaam na timu mchanganyiko ya Zanzibar na Chakechake,au Simba na Malindi ama Yanga na Miembeni na kadhalika.

Tatu,uwanja wa kumbukumbu ya Karume wa Ilala Dar es Salaam,ambao ndiyo wenye historia kubwa ya soka ya nchi hii,urudishwe kuwa wa kutumika kimashindano badala ya kugeuzwa wa mazoezi mazoezi,vimechi vidogo vidogo na makao makuu ya TFF! Unapaswa urudishwe kutumika kimashindano kwa mechi kadhaa kwa kutengenezewa majukwa ya kukaa watazamaji,jambo ambalo ni rahisi sana kufanyika kwa kuhusisha taasisi za kibiashara na kuingia mkataba nao wa kutengeneza majukwa hayo kwa makubaliano maalum ikiwemo kutangazia biashara zao uwanjani hapo.

Wakati mwingine tuwe tunafikiria kujenga.Tutakuwaje wahitaji wa maendeleo kwa kusubiri kila kitu tujengewe? Tujenge majukwaa ya uwanja wa Kumbu kumbu ya Karume ili miaka ijayo kwenye ligi kuu timu za Manyema Rangers,JKT Ruvu,Moro United,Azam na African Lyon zenye makao yake Dar es Salaam kimashindano ziutumie uwanja huo kama wa nyumbani zinapocheza na timu nyingine zote isipokuwa Yanga na Simba kama Mtibwa Sugar walivyo na Manungu na Jamhuri. Naomba ifanywe hivyo ili kulifanya jina la uwanja huo lilingane na ukubwa na umaarufu wa mtu mwenye jina hilo.

La mwisho, naomba sana historia iandikwe vizuri na kwa upande wangu naomba historia iwekwe sawa kuhusu jinsi Yanga na Simba zilivyoanzishwa,zilivyopata majengo yao na jinsi Simba ilivyobadilika toka kuwa Sunderland hadi kuwa Simba.Nimeeleza hapa kila nilicho na uhakika nacho lakini wangapi wataniamini? Naomba Mwenyezi Mungu azidi kuitunza mahala pema peponi roho ya Sheikh Abeid Aman Karume.Amen.

chanzo cha habari: sportsana.com

No comments