Mkiwagusa Twite, Dida patachimbika
KWANZA walisikia straika Didier Kavumbagu amesaini Azam FC
wakashituka, baadaye wakapotezea. Lakini Jumatano mchana waliposikia
Frank Domayo naye amesaini huko wakachanganyikiwa wakaitana ghafla
klabuni.
Hao ni wazee wa Yanga ya Dar es Salaam ambao
wametoa onyo kali na kusema kwamba wachezaji wao wote wawe huru
kuondoka, lakini endapo beki Mbuyu Twite na kipa Deo Munishi ‘Dida’
wakiondoka tu, patachimbika.
Wazee hao wamesisitiza kwamba wameupa uongozi
angalizo kwamba wafanye wanavyoweza wachezaji hao wasiondoke Yanga na
kama ikishindikana watazungumza mambo mengine.
Twite yuko kwenye mazungumzo na Azam ambapo
amewashinikiza Yanga wampe Sh80 milioni asaini mkataba mpya, jambo
ambalo viongozi hawakubaliani nalo kwa madai kwamba mchezaji huyo licha
ya kwamba ni kiraka lakini umri umemtupa.
Ndani ya wiki klabu ya Yanga imepata pigo kwa
kuchukuliwa wachezaji wake Kavumbagu na Domayo huku baadhi ya wanachama
wakionekana kuchanganyikiwa na kutoelewa ni nini kimetokea ingawa
Mwanaspoti linajua kwamba viongozi wa Yanga walizidiwa kete licha ya
harakati zao za kupambana.
Kavumbagu na Domayo wamesaini mikataba mipya ya
miaka miwili kila mmoja na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Azam hivyo wapo
tayari kuitumikia klabu hiyo msimu ujao wa ligi 2014/15.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu
wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali, alisema kuondoka kwa
wachezaji hao kumewashitua huku akisisitiza kuwa viongozi wa Yanga
wafanye kila wanaloweza kuhakikisha Twite na Dida wanabaki kwenye himaya
yao.
Akilimali ambaye ana ushawishi mkubwa kwa
wanachama wakongwe, alisema juzi Jumatano wazee walikutana katika Makao
Makuu ya klabu hiyo kujadili juu ya uchaguzi wao ujao pamoja na kufanya
tathimini ya ligi kuu msimu uliopita lakini kikao hicho hakikuweza
kumalizika baada ya kuingilia habari za usajili.
“Hawa wote waondoke tu, ila wazee tutaumia sana
endapo Twite na Dida wataondoka Yanga, sijui kilio chetu kitakuwaje na
sijui nini kitatokea ndani ya Yanga, hivyo viongozi wetu wafanye
wawezalo kuhakikisha wanawazuia wachezaji hao,” alisema.
Mbuyu Twite
“Tumeshika nafasi ya pili kwenye ligi jambo ambalo lilituhuzunisha sana, ila hatuwezi kulipinga kwani ndiyo mpira lakini sasa hivi tunaanza kupata picha kwamba huenda hata wachezaji hawakuwa na malengo, labda tayari walikuwa wameshawishiwa, hivyo waache waende tubaki na wale wazalendo na wataitumikia Yanga kwa moyo mmoja,” alisema Akilimali.
Akifafanua zaidi juu ya Twite, Mzee Akilimali
alisema kuwa “Twite ni mchezaji mwenye nidhamu kubwa na anajituma,
tunatamani angekuwa ndiye nahodha wa timu yetu ila haiwezekani kwa
sababu siyo raia wa Tanzania, Twite haonyeshi tamaa ya fedha anaonyesha
kipaji.
“Tumesikia Azam wanamtaka Twite ndiyo maana
tumeweka wazi kuwa viongozi wahakikishe anabaki kuichezea Yanga, bado
tunamuhitaji sana kutusaidia,” alisema Akilimali huku akisema wamesimama
kujadili mambo ya uchaguzi mpaka Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji
atakaporejea nchini.
Kutoka mwanaspot.
Kutoka mwanaspot.
No comments