SIMBA VS YANGA Huku mlokole Mwanjali, kule mbabe Bossou
NA ZAITUNI KIBWANA
HOMA ya mpambano wa watani wa jadi, Simba na Yanga unaotarajiwa
kuchezwa Oktoba mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, imezidi kupanda ambapo kila timu imejipanga kivyake kuhakikisha
inaibuka kidedea siku hiyo.
Kuelekea katika mchezo huo, makocha wa pande zote, Joseph Omog wa
Simba na Hans van der Pluijm wa Yanga, wamekuwa wakisuka vikosi vyao kwa
lengo la kupata matokeo mazuri na kuwafurahisha mashabiki wao.
Katika mpambano huo safu ya ulinzi kwa pande zote ndiyo inayoweza
kuamua matokeo ambapo Simba wanajivunia kuwa na Method Mwanjali ambaye
amecheza michezo yote sita iliyopita kwa ustadi mkubwa, huku Yanga wao
wakijivunia Vincent Bossou, ambaye hana masihara anapokutana na
washambuliaji wa timu pinzani.
Kwa ujumla mpaka sasa vikosi vya pande zote vimekamilika na hakuna
timu ambayo ina mchezaji muhimu mwenye majeraha ambaye anaweza kuukosa
mchezo huo mbali na Godfrey Mwashiuya wa Yanga ambaye amekuwa majeruhi
wa muda mrefu ambapo kazi itakuwa kwa makocha kuamua nani aanze na nani
aanzie benchi.
Katika kikosi cha Simba, idadi kubwa ya wachezaji wapo fiti na ni
wazi nafasi ya Vincent Angban langoni ipo wazi na kama kutakuwa na
tatizo lolote anaweza akapangwa Manyika Peter, huku Yanga wakijivunia
Ali Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’.
Mpaka sasa kipa wa Simba, Angban ameruhusu mabao mawili na ni kipa
ambaye tatizo lake kubwa ni kwamba si mzuri sana wa kuokoa mipira ya
krosi ikiwamo kona tofauti na akina Barthez na Dida wa Yanga.
Kwa upande wa beki wa kulia Simba inao Javier Bukungu, Malika Ndeule
pamoja na Hamadi Juma ambao wote wanatajwa kutokuwa na kasi kubwa ya
kupandisha mashambulizi na kurudi haraka kuokoa kama ilivyo kwa Juma
Abdul na Hassan Ramadhan ‘Kessy’ wa Yanga.
Simba wanajivunia kuwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kushoto huku
Yanga nao wakiwa na Haji Mwinyi, ambapo wote hao kazi yao inaonekana
huku mabeki wa kati shughuli ikiwa pevu ambapo Yanga wanajivunia Bossou,
Kelvin Yondani, Nadiri Haroub ‘Cannavaro’ pamoja na Andrew Vincent
‘Dante’, Simba wao wakiwa na Mwanjali, Novaty Lufunga na Jjuuko
Murushid.
Huenda Pluijm akawatumia Bossou na Dante kwani wameonyesha uelewano
mkubwa huku Omog akiumiza kichwa kati ya Lufunga na Jjuuko nani anacheza
sambamba na Mwanjali ambaye amekuwa nguzo kubwa ya Simba.
Safu hii ya ulinzi ya Simba imeruhusu mabao mawili huku ile ya Yanga
ikiruhusu kufungwa bao moja dhidi ya Stand United mchezo uliopita
walipopoteza mchezo huo kwa kufungwa bao 1-0.
No comments