MGOSI ASTAAFU SOKA
MSHAMBULIAJI mkongwe na nahodha wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi amestaafu rasmi soka na sasa anakuwa Meneja wa timu hiyo.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Manara
amethibitisha hilo na kusema Mgosi ataagwa rasmi katika mchezo wa
kirafiki kwa kimataifa utakaopigwa Jumapili ya juma hili uwanja wa Taifa
Dar es Salaam dhidi ya URA ya Uganda.
Manara ameeleza kwamba aliyekuwa Meneja wa timu, Abbas Suleiman Ally
anakuwa Mratibu wa timu (Team Coordinator) kuanzia leo na nahodha mpya
ni Jonas Mkude.
Aidha, kiungo wa klabu hiyo, Peter Mwalyanzi aliyesajiliwa msimu
uliopita akitokea timu ya Mbeya City FC, ametolewa kwa mkopo African
Lyon iliyopanda kucheza ligi Kuu msimu huu wa 2015/2016.
Simba wataingia kwenye mechi na URA wakiwapa nafasi mashabiki wao
kukiona kikosi chao kwa mara ya pili uwanja wa Taifa baada ya Agosti 8
mwaka huu siku ya Simba Day kuichapa 4-0 AFC Leopard ya Kenya.
Inaelezwa mechi na URA itakuwa ya mwisho ambapo Agosti 20 wataanza ligi kuu kwa kuchuana na Ndanda FC uwanja wa Taifa.
Lakini wakati huouo mtandao wa habari za michezo Mpenja Sports
umeripoti kwamba, mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya taifa Taifa
Stars, amekanusha taarifa za kutundoka daruga.
MPENJA SPORTS imemtafuta Mgosi na kumuuliza juu ya taarifa
hizo na maelezo yake ni haya: “Kwanza napenda kukanusha suala
lililoandikwa kwenye mitandao la Mgosi kustaafu, Mgosi kama Mgosi, suala
la kustaafu mpira bado sana, Pogba (Paul) atakapostaafu ndipo atafuatia
Mgosi kustaafu”. Amesema Mgosi na kuongeza”
Hata hivyo, Mgosi ameonesha wazi yuko tayari kufanya kazi yoyote
ndani ya Simba hata kama atakuwa nje ya uwanja, kitu kinachoashiria yuko
mbioni kutundika daluga.
“Mimi ni mchezaji wa Simba, ni Mfanyakazi wa Simba, nipo tayari
kufanya majukumu yoyote yanayoihusu Simba, aidha katika uchezaji au
sekta nyingine.”
Mgosi anayeheshimika ndani ya Simba amesema kutekeleza majukumu
mengine nje ya kucheza ndani ya Simba alishaanza msimu uliopita, lakini
hakuna aliyehusisha na kustaafu soka.
“Kuisaidia Simba nje ya uwanja nimelifanya hilo toka mwaka jana,
lakini mbona halijaandikwa hivyo, mwaka jana nimekuwa msaidizi wa
Mayanja (Jackson), nilimsaidia kila kitu kama kocha msaidizi”.
Amesisitiza Mgosi na kufafanua: “Unapozungumza mtu kistaafu tuwe na
subira, lazima niseme mwenyewe, sio mitandao iandike, wengine wanaandika
wapate comments, likes na kushtusha watu ambao wananihitaji.”
MPENJA SPORTS imemuuliza kama anaamini muda wa kustaafu umefika na yuko tayari kuwa Meneja wa Simba.
“Sio tatizo, ni jukumu ambalo nitalifanyia kazi kwa vile
ninavyofahamu mimi, ukitaka kuangalia kiongozi anayeweza kuingoza Simba
kwa kila kitu, hakuna mtu ambaye kwa haraka unaweza kumuangalia zaidi ya
Mgosi, kwasababu ni mtu ninayeheshimika na wachezaji, naheshimika na
mashabiki, naheshimika na viongozi wa Simba, naamini katika sekta yoyote
nitakayopewa Simba, hakuna atayepinga, kwahiyo najivunia klabu yangu ya
Simba,” ameongeza Mgosi.
Licha ya kakanusha kustaafu rasmi, taarifa za ndani ambazo MPENJA
SPORTS imezipata ni kuwa kweli Mgosi anaelekea kustaafu na mechi ya
Jumapili dhidi ya URA itakuwa maalum kwake kuagwa, lakini yeye mwenyewe
na uongozi hauko tayari kulizungumzia kwasababu kuna masuala kadhaa
wanajadiliana.
Inaelezwa keshokutwa Jumamosi, Mgosi atakutana na viongozi wa Simba
kujadili suala la nafasi wanayotaka kumpa ikiwemo kuandaa mkataba .
No comments