Tupashane Habari 24-hours

Tupashane Habari 24-hours

Breaking News

kampa kampa tena

Yanga yajichanganya CAF

HUSSEIN OMAR NA SALHA HASHIM, RCT

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, klabu ya Yanga ya Dar es Salaam imejichanganya katika usajili wake wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu baada ya kutuma namba tofauti za wachezaji wake.
Picha kamili iko hivi: Siku zote Amissi Tambwe anavaa jezi namba 17, lakini makosa yaliyofanywa na uongozi wa timu yake umesababisha avae jezi namba 19 katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, jezi ambayo inamilikiwa na Geoffrey Mwashiuya ambaye amelazimika kutumia jezi namba 29 katika michuano hiyo.
Kwa mujibu wa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, kosa hilo lilifanyika wakati Katibu Mkuu wa zamani wa timu hiyo, Jonas Tiboroha, alipokuwa akituma majina ya kikosi cha miamba hiyo kwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambapo hakujua kuwa Mwashiuya na Tambwe walishabadilisha namba na kujikuta akituma namba zao za zamani.
“Unajua Tambwe alivyofika Yanga alikuta jezi namba 17 inavaliwa na Mrisho Ngassa,” alisema Hafidh. “Ikabidi yeye achukue jezi namba 19, wakati Mwashiuya kwa upande wake tulimkabidhi jezi 29.
“Ila baada ya Ngassa kuondoka, Tambwe alikuja kwangu na kuomba jezi namba 17 nikampa, huku Mwashiuya naye akichukua namba 19, lakini wakati Tiboroha anapeleka majina hakuwasiliana na mimi hivyo hakujua kama wachezaji hawa wameshabadilishana jezi.”
Hafidh aliongeza kusema wameshindwa kuwabadilishia namba wachezaji hao kwa sababu mchakato wa kufanya hivyo ni mrefu sana na ndiyo maana wamewaacha waendelee kutumia namba hizo kwenye michuano ya kimataifa.
Yanga imetinga raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa ya Cercle de Joachim ya Mauritius kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-0 na sasa itakutana na APR ya Rwanda katika hatua hiyo.

No comments