Mourinho awachana wachezaji wake.
Baada ya kupoteza mchezo mwingine kwenye michuano ya ligi ya mabingwa ukiwa mchezo wa tano kupoteza tangu msimu huu uanze , hali imezidi kuwa mbaya ndani ya klabu ya Chelsea kufuatia mkutano ambao kocha Jose Mourinho aliufanya na wachezaji wake .
Katika mkutano huo inasemekana Mourinho aliwashutumu wachezaji wake akiwataja baadhi kwa majina kwa kile ambacho alikiita kuonyesha kiwango duni ambacho hakiendani na hadhi ya klabu yao .
Mourinho amekuwa mbogo msimu huu akiwalaumu wachezaji wake kinyume na ambvyo alikuwa akifanya msimu uliopita wakati klabu hiyo iliposhinda ubingwa wa ligi kuu ya England ambapo kocha huyo alionekana kuwa mpole na muelewa.
Katika mkutano uliofanyika kwenye makao makuu ya klabu siku ya jumatano baada ya timu kurudi toka Ureno ambako walifungwa na Fc Porto Mourinho aliwashutumu vikali wachezaji wake kwa kiwango kibovu na alifikia hatua ya kutishia mkuwapanga wachezaji wa kikosi cha pili .
Hali hii imetafsiriwa na wengi kuwa ni shinikizo kubwa ambalo Mourinho anakumbana nalo msimu huu kutokana na Chelsea kushindwa kufanya vizuri kama ilivyokuwa msimu uliopita .
Mourinho aliwashutumu wachezaji kama Caesar Azipilicueta, Branislav Ivanovic na Nemanja Matic ambapo alimwambia wazi Matic kuwa amekuwa kwenye kiwango kibovu na anahitaji kufanya mazoezi ya ziada.
Mourinho hakumuacha beki Caesar Azpilicueta ambaye alimwambia kuwa ana bahati kubwa kuwa Chelsea haina beki wa kushoto asilia na kama ingekuwa hivyo asingepangwa kwenye kikosi cha kwanza.
Hadi sasa Chelsea imejikuta kwenye wakati mgumu baada ya mfululizo wa matokeo mabaya huku Mourinho akizidi kuwa na uhusiano mbovu na baadhi ya wachezaji wake akiwemo nahodha John Terry ambaye amekuwa akiwekwa benchi .
Source: Millard Ayo
No comments