YANGA WALIKUWA ‘JAMVI LA WAGENI’ 1998, SASA WATAKUWA WABABE WA AFRIKA
Na Baraka Mbolembole
Mabingwa mara mbili mfululizo wa ligi kuu Tanzania Bara, timu ya
Yanga SC imekuwa timu ya kwanza Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya,
Uganda, Rwanda na Burundi) kufuzu kwa hatua ya makundi katika michuano
ya Shirikisho Afrika.
Yanga ilikuwa timu ya kwanza pia ukanda huu kufuzu kwa hatua ya
makundi ya ligi ya mabingwa Afrika mwaka 1998. Ni wa kwanza katika kila
kitu na licha ya kupoteza game ya marejeano jana Jumatano huko mjini
Dundo, Angola dhidi ya wenyeji wao Esperanca, mabingwa hao mara 26 wa
kihistoria Tanzania Bara wamefanikiwa kukata kiu ya mashabiki wao na
wadau wa kandanda Tanzania ambao wamekuwa wakilalamika namna klabu ya
VPL zinavyoshindwa mapema katika michuano ya CAF kila mwaka.
Timu ya mwisho ya Tanzania na Afrika Mashariki kufuzu kwa hatua ya
makundi ya michuano ya CAF ni Simba SC ambayo inakumbukwa namna
walivyowavua ubingwa wa ligi ya mabingwa Zamalek ya Misri na kufuzu kwa
hatua ya makundi mwaka 2003. Miaka 13 Leo, Yanga wamefanya hivyo tena,
japokuwa safari hii ni katika michuano ya Shirikisho.
Wakati ule (1998) walipofuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza
katika ligi ya mabingwa, Yanga walipangwa katika kundi moja na Asec
Mimosas ya Ivory Coast, Manning Rangers ya Afrika Kusini, na Raja
Casablanca ya Morocco. Kwa wakati huo, Asec na Raja zilikuwa timu tishio
sana katika michuano ya CAF hivyo Yanga ni kama waliangukia katika
‘kundi la kifo’ na kilichowakuta katika michezo 6 ya makundi hawapendi
kabisa kukikumbuka.
Waliishia kupewa jina ‘Jamvi la Wageni’ kwa maana game yao ya kwanza
tu dhidi ya Raja walikutana na kipigo cha ‘mbwa mwizi’ kutoka kwa Raja
baada ya kuchapwa 6-0, Casablanca, wakapigwa 3-0 na Asec katika uwanja
wa Uhuru, wakaenda Afrika Kusini wakapigwa 4-0 na Manning Rangers.
Walipoteza pia ugenini 2-1 dhidi ya Asec. Matokeo 1-1 dhidi ya
Manning na 3-3 dhidi ya Raja katika uwanja wa Uhuru yalikuwa mazuri
zaidi kwao katika michezo 6 ambayo walimaliza wakiwa wameruhusu magoli
19 na kufunga magoli matano tu. Hili halitajirudia na Yanga haitakuwa
tena ‘jamvi la wageni’ katika michuano ya CAF.
FUS Rabat, Kawkab Marrakech zote za Morocco, Etoile du Sahel ya
Tunisia, Ahli Tripoli ya Libya na MO Bejaia ya Algeria, Medeama ya Ghana
na TP Mazembe ya Jamhuri ya DRC ni timu nyingine 7 ambazo zinasubiri
kupangwa katika makundi mawili ya michuano hiyo. Yanga imepiga hatua
sana ndani ya uwanja, katika utawala na mashabiki wanatembea kwa
majigambo kwa kuwa wanaona kazi inayofanywa na timu yao.
Yanga SC ilikuwa ‘jamvi la wageni’ 1998, sasa watakuwa wababe wa
michuano kwa maana wana timu nzuri, kocha mzuri, uongozi mzuri, na timu
kiumjumla ni bora. Yanga haitaishia hatua ya makundi tu, imani yangu ni
itasonga mbele zaidi ya hapo na watavunja rekodi zao wenyewe. Hongera
sana Yanga SC kwa kufuzu hatua ya makundi Shirikisho Afrika.
Source:
No comments