Tupashane Habari 24-hours

Tupashane Habari 24-hours

Breaking News

kampa kampa tena

YANGA HII HAITABIRIKI.


YANGA hii ya sasa haitabiriki katika suala zima la ufungaji mabao kwani hakuna mchezaji maalumu ambaye anaweza kutajwa kuwa mwenye jukumu la kucheka na nyavu.
Katika mechi saba zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika, wachezaji tofauti wameifungia mabao timu hiyo inayonolewa na Mholanzi, Hans van der Pluijm.
Ndani ya mechi hizo, wachezaji sita katika kikosi hicho walifanikiwa kufunga mabao hali inayotoa picha kuwa Yanga imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kujenga mfumo bora wa ufungaji.
Wachezaji ambao tayari wameshacheka na nyavu za wapinzani katika kikosi cha Yanga, ni beki wa kati na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, winga wa kushoto Mbrazil, Andrey Coutinho, winga wa kulia, Simon Msuva, washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe na Mrisho Ngassa.
Lakini pia katika mechi za nyuma, kuna wachezaji kama mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman ambaye naye alifunga katika michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar, lakini pia washambuliaji, Danny Mrwanda na Jerry Tegete ambao nao walicheka na nyavu.
Watatu hao ukiwajumuisha na sita waliofunga katika mechi za hivi karibuni, ninatoa majibu kuwa ndani ya kikosi cha Yanga hakuna mchezaji anayeweza kutabiriwa kuwa ndiye atakayefunga katika mechi yoyote, iwe ni ya Ligi Kuu Bara au Kombe la Shirikisho.
Lakini kwa kiasi kikubwa matokeo hayo yote yanatokana na ujio wa Pluijm ambaye amekuwa akisifika kwa kufundisha soka la kushambulia kwa muda wote.
Kwa bahati nzuri, Mholanzi huyo amefanikiwa kuwa na kikosi cha wachezaji wenye uwezo wa kumudu soka la mashambulizi na wakati huo huo kurudi kujilinda.
Miongoni mwa vitu vinavyoibeba Yanga katika mfumo huo, ni kuwa na mawinga wenye kasi ya kuwawezesha kufanya mashambulizi na kurudi kuzuia, lakini pia takribani viungo na washambuliaji wake wote wana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira hali inayowafanya kuwa vigumu kupoteza mpira ovyo.
Takwimu zinaonyesha ndani ya mechi saba zilizopita, Yanga imefunga mabao 14, lakini wao wakiruhusu nyavu zao kutikishwa mara tatu tu.
Tayari Pluijm ameweka wazi jinsi alivyo na imani kubwa na washambuliaji wake, lakini pia na wengineo wakiwamo mabeki na viungo ambao wameonyesha uwezo wa kufunga mabao pale walipopata nafasi.
Katika mazoezi yake, amekuwa akiwajenga wachezaji wote kuwa na uwezo wa kufunga ili inapotokea mshambuliaji fulani anakabwa kwa karibu na mabeki wa timu pinzani, hali hiyo itoe mwanya kwa wengine kucheka na nyavu.
Mfumo huo kwa kiasi kikubwa ndio ulioonekana kuiponza Tanzania Prisons jijini Mbeya Alhamisi ya wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Sokoine, ambapo wakati wakiingia uwanjani kwa kukamia kuwakaba Tambwe na Ngassa walioifunga BDF XI katika mchezo wa Kombe la Shirikisho, walishtukia nyavu zao zikitikiswa mara tatu na Msuva na Coutinho.
Katika mchezo wa juzi Jumapili, Msuva alifunga bao moja na mengine kufungwa na wachezaji wengine ambao ni Tambwe na Ngassa.
Hali hiyo ndiyo inayowafanya wachambuzi wa soka nchini kuitabiria makubwa Yanga kwamba ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na makali yake katika suala zima la ufungaji mabao.

No comments